Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA), Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 2023.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ametoa taarifa hiyo leo alipofanya mahojiano na mwandishi wa Habari Leo, akieleza kuwa alimuomba Rais Samia naye ameridhia ombi hilo.
“Siku zote anawasikiliza wakina mama wa chama chake, tulimuomba aje awaone atambue kazi kubwa inayofanywa na akina mama wa Chadema kwa hiyo Rais atakuwa mgeni rasmi katika tukio letu na mimi nitakuwepo kumpokea,” alisema Mbowe.
Ameeleza kuwa mkutano huo utafanyika mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na wanawake wa vyama mbalimbali vya siasa.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kuhudhuria tukio la kisiasa la chama kikuu cha upinzani.
Rais Samia ameendelea kuweka rekodi, ikikumbukwa kuwa alihudhuria tukio la muziki lililoandaliwa na mbunge wa zamani wa Mbeya ambaye ni kiongozi wa Chadema, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi.