Mkuu wa Mawasiliano na Itifaki wa Umoja wa Posta Afrika – PAPU, Faustine Oyuke amesema Mkoa wa Arusha unatazamiwa kuwa Kitovu cha Wataalamu wa Sekta ya Posta barani Afrika baada ya uwepo wa jengo la kisasa la Umoja huo litakalozinduliwa na Rais Dkt. Samia Septemba 2, 2023.
Akizungumza jana jijini humo, Oyuke amesema Umoja wa Afrika umejenga jengo hilo ukilenga kuboresha Sekta ya Posta na kukuza uchumi wa kidijitali, likiwa na huduma mbalimbali ikiwemo taasisi za fedha na kumbi za mikutano.
Amesema, “ jengo hili litakuwa kitovu cha taaluma ya Sekta ya Posta kwasababu kuna ukumbi maalum wa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa wataalamu wa Sekta ya Posta barani Afrika ambao ni nchi wanachama na marafiki wa umoja huo ili kuja kujifunza kwa namna gani sekta hiyo inakuwa chachu ya maendeleo barani Afrika.”
Aidha, Oyuke ameongeza kuwa katika jengo hilo kutakuwa na Ofisi za Umoja wa Posta Afrika ambazo zitakuwa katika ghorofa tatu za 13, 14 na 15 na Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA, Kanda ya Kaskazini.