Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kifo cha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhandisi Elias Kwandikwa, kimeacha pengo kubwa kwa serikali kwani alikuwa kiongozi mwadilifu na anayependa kujifunza kila siku.
Ameysema hayo leo Agosti 6, 2021 katika viwanja vya Karimjee alipohutubia baada ya ibada ya kumalizika na kuongoza viongozi mbalimbali kuaga mwili wa Marehemu Elias John Kwandikwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na kujenga Taifa.
“Kifo cha Kwandikwa kimeacha pengo sio tu kwa familia bali pia kwenye serikali, hadi mauti yanamkuta alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hivyo ni wazi kifo chake ni pigo kwa serikali,” Amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kipindi akiwa Makamu wa Rais, marehemu Elias Kwandikwa alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na walifanya kazi kwa karibu hasa walipokuwa na ziara katika mikoa mitatu Singida, Tabora na Shinyanga.
“Tulianza Singida, tukaenda Tabora, tukamalizia Shinyanga, katika ziara hiyo alikuwa makini na mfuatiliaji, mtulivu na msikivu na asiye na makuu, hakuwahi kutoa sababu ya kutoka nje ya ziara mpaka tumemaliza,” Amesema Rais Samia.
Amesema sababu hizo zilipelekea yeye (Rais Samia) na Hayati Dkt. John Magufuli kumteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na mwaka 2020 kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Waziri Elias Kwandikwa alifariki dunia Agosti 2, 2021 jijini Dar es Salaam na atazikwa kijijini kwao Ushetu, Kahama Agosti 9 mwaka huu.