Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis amewahasa Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na watoa huduma katika sekta ya Afya nchini kuhakikisha wazee wanapewa kipaumbele katika kupata huduma ya chanjo ya ugonjwa wa Uviko -19.

Ametoa kauli hiyo leo August 5,2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisisitiza wazee ni kundi ambalo lipo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya Uviko 19 hivyo  wanastahili kulindwa ili kuimarisha ulinzi na usalama wa afya zao.

“Kwa kuwa uzee na kuzeeka unaambatana na upungufu wa kinga ya mwili, Serikali inatoa wito kwa wazee wote nchini kujitokeza kwa wingi kutumia fursa ya chanjo ya UVIKO 19 inayotolewa bure katika vituo mbalimbali vilivyoainishwa,” Amesema Mwanaidi.

Aidha ameyataka Mashirika na Asasi za kiraia zinazotoa huduma kwa wazee kuandaa na kuendesha Programu mbalimbali za kuhamasisha wazee kwenda kupata chanjo ya UVIKO 19 kwa hiari yao ili kuimarisha kinga katika miili yao.

Hata hivyo Naibu Waziri wa Afya anaeshughulikia Maendeleo ya jamii Mwananidi, ameisisitiza jamii kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia miongozo kutoka kwa wataalamu wa afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi na tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Shilungu Ndaki, amesema kuwa Serikali itahakikisha kundi la wazee linasimamiwa vizuri katika kupata huduma ya chanjo ya UVIKO 19 ili kulilinda kundi hilo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.

RC Makalla azindua Kampeni ya usajili wa walipakodi
TBS imeiingizia serikali bilioni 3.9 ukaguzi wa magari