Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Ismail Rage amempongeza Rais wa Shirikisho la soka Tanzania ‘TFF’, Wallace Karia kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kulipa hadhi na thamani soka la Tanzania.
Rage ambaye pia aliwahi kuhudumu nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama ha Soka Tanzania ‘FAT’ kwa sasa ‘TFF’ amesema muda mfupi ambao kiongozi huyo amekaa madarakani amefanya mambo makubwa kuliko viongozi wote waliopita tangu uhuru.
“Kama kuna kitu Watanzania wapenda soka tunatakiwa tujivunie ni kumpata Karia, ni Rais bora kuwahi kutokea kwenye mpira tangu tupate uhuru, sijaona kama yeye, nimekuwepo FAT na TFF tulishindwa kumleta Issa Hayatou wala Sepp Blatter hadi wameondoka madarakani.” amesema Rage
Kiongozi huyo amesema kwa Karia imekuwa tofauti kwani kwa muda mfupi aliopo madarakani Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, Patrice Motsepe amekuja nchini mara tatu sawa na Rais wa FIFA Gianni Infantino.
Rage amesema mbali na ujo wao viongozi hao wakubwa wa mpira Afrika na Duniani lakini pia misaada inakuja nhini ikiwemo kozi za makocha kwa madaraja mbalimbali, miradi ya miundombinu ya TFF na matumizi yake yanaonekana.
Amesema anashangazwa na baadhi ya watu kutoyaona hayo ndio maana inapotokea ratiba ya ligi inakuwa na viporo vingi au mwamuzi amefanya makosa kwenye kutoa maamuzi TFF ndiyo inatupiwa lawama wakati inayohusika na mambo hayo ni Bodi ya Ligi ‘TPLB’.