Mwenyekiti wa Kampuni ya beIN, na Rais wa klabu bingwa nchini Ufaransa PSG Nasser Al-Khelaifi, anashtakiwa kwa kosa la kumshawishi Katibu mkuu wa zamani wa shirikisho la soka duniani *FIFA* Jerome Valcke, kutenda kosa la jinai na kupokea rushwa.
Mwenyekiti huyo wa Shirika la Habari la BeIN lililoko huko Qatar, ambaye pia ni afisa mwandamizi wa FIFA amekwenda kwenye kesi nchini Uswizi akituhumiwa juu ya kupokea rushwa katika utoaji wa haki za matangazo ya Televisheni kwa ajili ya fainali zijazo za Kombe la Dunia (2022).
Al Khelaifi, ambaye yupo pia kwenye kamati kuu ya bodi ya soka ya Shiruikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA), ameshtakiwa kwa kumshawishi Valcke kupokea kiasi cha zaidi ya dola za kimarekani milioni moja.
Valcke mwenye umri wa miaka 59, ambaye tayari amefungiwa na kamati ya maadili ya FIFA kwa miaka 10, kwa ukiukaji wa maadili alifika Mahakamani Jumatatu akituhumiwa kupokea rushwa, kufanya usimamizi mbaya na kughushi nyaraka.
Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka ya jinai juu ya madai kwamba Valcke alitumia nafasi yake kushawishi utoaji wa haki za matangazo ya TV kwa Italia na Ugiriki kwenye fainali kadhaa za Kombe la Dunia na Kombe la Mabara tangu mwaka 2018 hadi 2030.
Waendesha mashtaka wa Uswizi wamekuwa wakichunguza ufisadi unaozunguka Fifa tangu 2015, kipindi shirikisho hilo la mpira wa miguu ulimwenguni lilipokuwa likiingia katika kashfa mbaya zaidi ya ufisadi katika historia yake.
Kashfa hiyo ilisababisha Rais wake Sepp Blatter na Rais wa UEFA Michel Platini kufungiwa maisha kwenye mchezo huo, wakati maafisa kadhaa walishtakiwa nchini Marekani kwa tuhuma zinazohusiana na ufisadi.