Mchezaji wa timu ya Taifa ya Ujerumani na Klabu ya Arsenal, Mesut Özil amefunga ndoa na aliyekuwa mchumba na kusimamiwa na Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan.
Ozil amefunga pingu za maisha Ijumaa, Juni 7, 2019 na Amine Gulse, aliyewahi kushinda taji la urimbwende wa nchi hiyo (Miss Turkey). Hatua hiyo imeifanya harusi hiyo kuwa maarufu zaidi na kuhudhuriwa na watu wengi mashuhuri.
Wapendanao hao walianzisha uhusiano wao mwaka 2017 na wakatangaza kuwa wachumba Juni 2018. Machi mwaka huu, Ozil aliweka wazi kuwa amemuomba Rais Erdogan awe msimamizi wa ndoa yao.
Hata hivyo, ombi la Ozil lilipingwa vikali na watu wasiomuunga mkono Rais Erdogan wakiwemo viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya Ujerumani.
Ozil ambaye alizaliwa Gelsenkirchen, Ujerumani alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake kupata mafanikio katika Mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2014, lakini mwaka jana alikuwa sehemu ya kikosi kilichopata pigo kwenye mashindano hayo.
Amekuwa akipigiwa kura za kuwa mchezaji bora wa timu ya Taifa mara tano tangu mwaka 2011 na anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji bora zaidi duniani.
Ozil na mkewe Gulse ambaye alivishwa taji la Miss Uturuki 2014, walitoa mchango wa chakula kwa wakimbizi 15,000 wa Syria.