Mahakama nchini Comoros imemuhukumu kifungo cha maisha gerezani bila kukata rufaa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Ahmed Abdallah Sambi kwa uhaini.
Sambi alipatikana na hatia ya kuuza hati za kusafiria za Comoros kwa watu wasio na uraia wa taifa hilo na wanaoishi katika mataifa ya Ghuba na pia ameshtakiwa kwa ubadhirifu wa mamilioni ya dola.
Sambi (64), alikataa kuhudhuria vikao katika Mahakama ya Usalama ya Taifa ambayo maamuzi yake hayawezi kukatiwa rufaa.
Rais huyo wa zamani wa Comoro ambaye ni mpinzani mkuu wa Rais Azali Assoumani tayari alikuwa amekaa gerezani kwa miaka minne kabla ya kukabiliwa na kesi.
Sambi, aliongoza taifa hilo la visiwani kati ya mwaka 2006 na 2011, alipitisha sheria mwaka 2008 inayoruhusu uuzaji wa hati za kusafiria kwa ada ya juu, Wakili wake alisema hakuna ushahidi wa kupotea kwa pesa.