Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi (Bara), Joseph Selasin ameiomba Mahakama Kuu Masjala Kuu, imuongezea muda ili aweze kuwasilishwa nyaraka za utetezi.

Selasini amefunguliwa kesi mahakamani hapo na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia akimtaka amlipe Sh3 bilioni kwa madai amemdhalilisha.

Maombi hayo madogo namba 541/22 yamewasilishwa mahakamani hapo leo Jumanne Novemba 29, 2022 na Wakili wa utetezi, Hassan Mkwanya mbele ya Jaji Obadia Bwegoge.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia akitoka Mahakama Kuu Masjala Kuu baada ya kesi kuahirishwa

Wakili Mkwanya amedai Novemba 23, 2022 alipokea maelekezo ya kumwakilisha Selasini ambapo ilikuwa ni nje ya muda unaotakiwa kuwasilisha utetezi kisheria.

“Nilipoangalia nilikuta siku 21 za kuwasilisha utetezi kisheria zimepita, tukaona tuwasilishe maombi ya kuongezewa muda kwaajili ya kuleta utetezi,” alidai Wakili Makwanya.

Wakili wa Mbatia, Hurdson Mchau alidai siku 21 zimeisha tangu Novemba 18 na Wakili wa utetezi alipata taarifa hiyo Novemba 23, hata nakala ya maombi hawajaiona na kuiomba mahakama kupanga tarehe ya karibu ili kuona maombi hayo yana sababu za msingi.

Hata hivyo, Jaji Bwegoge ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, 2023 kwaajili ya kusikiliza maombi ya Selasini kama sababu za kuomba kuongezewa muda ni za msingi au la.

Katika kesi hiyo ya msingi namba 184/2022, Mbatia anaiomba mahakama itamke kuwa tuhuma alizozitoa Selasini dhidi yake ni za uwongo, imwamuru amuombe radhi hadharani na kisha amlipe fidia ya Sh3 bilioni.

Majaliwa awapa maelekezo DAWASA
Rais wa zamani wa Comoro ahukumiwa maisha kwa wizi