Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta leo, Februari 4, 2020 ametangaza kuwa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Daniel Arap Moi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Kenya imeeleza kuwa Moi alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Nairobi tangu Oktoba 2019 na kwamba hakuwahi kutoka katika hospitali hiyo hadi alipofariki dunia.
Kwa mujibu wa msemaji wa Rais Kenyatta, Lee Njiru, Moi alikuwa akihudhuria matibabu katika hospitali hiyo kama mgonjwa wa nje kwa kipindi kirefu hadi alipolazwa Oktoba 2019.
Alisema afya ya Moi ilianza kudhoofika miaka mitatu iliyopita, akianza kutembea kwa kutumia fimbo hadi alipoanza kutembea kwa kutumia baiskeli ya miguu mitatu (wheelchair).
Ingawa Moi alikuwa na afya nzuri wakati na baada ya kipindi cha urais wake, Januari 2017 alianza kupata tatizo la goti na kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan kutokana na ajali ya gari aliyoipata mwaka 2006.
Machi 2018, mtoto wake wa kiume, Gideon na daktari wake, David Silverstein walimsindikiza nchini Israel kwa kile walichoeleza kuwa wanaenda kufanya vipimo vya kawaida katika goti alilofanyiwa upasuaji.
Mwaka mmoja baadaye, Rais huyo wa zamani wa Kenya alilazwa katika Hospitali ya Nairobi na hapo alifanyiwa pia vipimo zaidi. Oktoba 2019, kulikuwa na ripoti kuwa amelazwa katika hospitali hiyo lakini msemaji wake alikanusha hizo taarifa. Baadaye, Ikulu imeeleza kuwa ni kweli alilazwa katika kipindi hicho.
Ingawa afya yake haikuwa imara sana katika kipindi hiki cha miaka ya hivi karibuni, nguli huyo wa siasa aliendelea kupokea wageni wengi nyumbani kwake, wengi wakiwa wanasiasa wakubwa wa nchi hiyo na nje ya nchi waliotaka ushauri.
Waliofika nyumbani kwa Moi hivi karibuni kwa ajili ya ushauri ni pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, Gavana wa Mombasa, Hassan Joho na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir.
Moi aliiongoza Kenya kwa kipindi cha miaka 23 kuanzia Oktoba 14, 1978 – Desemba 30, 2002.