Rais wa zamani wa Misri, Mohammed Morsi amefariki dunia leo baada ya kuanguka ghafla akiwa mahakamani alipokuwa akisikiliza kesi inayomkabili tangu aondolewe na jeshi mwaka 2013.
Morsi ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la Islamic Brotherhood lililopigwa marufuku muda mfupi baada ya kumuondoa madarakani, alihukumiwa kifo kwa makosa ya ugaidi lakini mwaka 2016 mahakama ilibatilisha hukumu hiyo.
Morsi mwenye umri wa miaka 67, aliingia madarakani kupitia uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo mwaka 2012, lakini mwaka mmoja baadaye aliondolewa na jeshi kutokana na maandamano makubwa ya kumpinga yaliyozuka.
Mwanasiasa huyo amekuwa mahabusu tangu mwaka 2013 na leo alikuwa amepandishwa kizimbani kusikiliza mashtaka ya ugaidi yaliyotokana na tuhuma za kufanya mawasiliano na kundi la Hamas la Pakistan, kwa mujibu wa kituo cha runinga cha taifa hilo.
Alizaliwa mwaka 1951 katika kijiji cha El-Adwah katika Jimbo la Nile Delta. Alichukua masomo ya uhandisi katika Chuo Kikuu cha Cairo miaka ya 1970; na baadaye alienda Marekani ambapo alisoma na kuhitimu Shahada ya Udaktari wa Falsafa (Phd).
Mwaka 2012, alichaguliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Muslim Brotherhood na alifanikiwa kushinda hasa baada ya kuahidi kuwa ataunda ‘Serikali ya watu wote’.
Baada ya mwaka mmoja, wapinzani wake walifanikiwa kutengeneza vuguvugu lililosababisha maandamano makubwa kisha Jeshi likamuondoa madarakani na kumuweka mahabusu ambapo alikabiliwa na kesi nzito za ugaidi. Serikali iliyoingia madarakani iliwasaka na kuwakamata wafuasi wa Morsi na kupiga marufuku ‘Muslim Brotherhood’.