Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema amesitisha utumishi wa maofisa mbalimbali wa serikali pamoja na mabalozi akiwemo Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Balozi Benson Chali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msaidizi Maalumu na Msemaji wa Rais wa Zambia, Anthony Bwalya, Rais Hichilema amesitisha utumishi wa viongozi hao ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake ya kuwa na viongozi wanaowatumikia wananchi.
“Rais Hichilema anaeleza kwamba kusitishwa kwa utumishi wa baadhi ya maofisa wa serikali ni muhimu ili kupandikiza utamaduni mpya wa uwajibikaji kwa namna ambayo serikali inavyofanya kazi katika ngazi ya ukatibu mkuu na ngazi nyingine za juu serikalini,” amesema Bwalya katika taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kwamba Rais Hichilema amesitisha utumishi wa baadhi ya mabalozi wanaoiwakilisha Zambia katika mataifa mbalimbali ili kujenga utamaduni mpya wa diplomasia ya uchumi inayozingatia weledi.
Amesitisha utumishi wa mabalozi 13 ambao ni Chali (Tanzania), Anthony Mukwita (Ujerumani), Emmanuel Mwamba (Ethiopia), Martha Lungu (Uswisi), Profesa Nkandu Munalula (Ubelgiji) na Paul Mihoba (Uingereza).
Wengine ni Winnie Chibesakunda (China), Judith Kapijimpanga (India), Emmanuel Chenda (Zimbabwe), Daniel Chisenga (China), Alfreda Kasembe (Brazil), Ibrahim Mumba (Saudi Arabia) na Goodwell Lungu (Botswana).
Hichilema alifanikiwa kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 12 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Rais Lungu, ambaye alikuwa akitetea nafasi yake kwa muhula wa pili.
Tangu alipoapishwa kuliongoza taifa hilo lenye utajiri wa madini ya shaba, Hichilema amekuwa akifanya mabadiliko katika serikali yake kwa kuwaondoa washirika wa Lungu ambao anasema wengi wao walishindwa kusimamia maslahi ya wananchi.