Vinara wa Kundi C katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Raja Casablanca, wameingia majaribuni katika Michezo ya Michuano hiyo, baada ya kubaini hujuma nzito wanazofanyiwa.

Raja Casablanca mwishoni mwa juma hili itaikaribisha Horoya AC ya Guinea mjini Casablanca-Morocco, kwa mchezo wa mzunguuko wa Tatu wa Kundi C, ambao umepangwa kupigwa Uwanja wa Mohamed V, chini ya Mwamuzi Peter Waweru kutoka Kenya.

Taarifa ambazo zimetufikia katika Dawati la Habari za Michezo Dar24 Media, kutoka ndani ya Klabu ya Raja Casablanca, zinamtaja Rais wa Shirikisho la Soka nchini Morocco Fouzi Lekjaa, kuihujumu Raja Casablanca ili isifuzu hatua ya Robo Fainali.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa Rais Fouzi ambaye ni Rais wa Klabu ya RS Berkane, amekua akishirikiana na baadhi ya Viongozi Wydad Casabanca, kuhakikisha Raja Casablanca haifanikiwi katika harakati zake za kufuzu Robo Fainali ikitokea Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu.

Inadaiwa kuwa mpango mkakati wa hujuma dhidi ya Raja Casablanka ulioandaliwa na Rais Fouzi pamoja na jopo lake, umebainika na tayari andiko limeachiwa hadharani huko nchini Morocco.

“Ndio kama unavyoona tunajaribu kuiwakilisha Morocco kama klabu Bora na yenye viwango, lakini huyu jamaa kwa sababu ni Rais wa timu nyingine huko Morocco (RS Berkane) na rafiki yake ni Rais wa timu nyingine (Wydad) hawataki kuona tunacheza vizuri na kutwaa ubingwa wa Afrika.”

“Ni ujinga, ametuwekea mazingira magumu katika Ligi ya Morocco (anatuhumiwa kutoa rushwa kwa waamuzi na kwa timu nyingine ili tupoteze michezo yetu) na alifanya vivyo hivyo kwenye Ligi ya mabingwa Barani Afrika msimu uliopita, tulipocheza dhidi ya Al Ahly ya Mirsi, Mwamuzi alitufanyia kusudi na tukatolewa hatua ya Robo Fainali.”

“Alipigania sana Fainali kuchezwa hapa Morocco, ili kuhakikisha wenzetu Wydad Casablanca wanakuwa sehemu ya timu zitakazocheza hatua hiyo, pia alishikilia msimamo ndani ya CAF, akitaka mchezo mmoja wa Fainali kuchezwa katika Uwanja wa Mohamed V, dhidi ya Al Ahly na alifanikiwa.” imeeleza taarifa iliyotumwa Dar24 kutoka Morocco.

Mbali na kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Morocco Fauzi, pia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ baada ya Rais Patrice Motsepe.

Hadi sasa Raja Casabanca wanaongoza msimamo wa Kundi C, wakimiliki alama sita, baada ya kuzifunga timu kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ Vipers SC ya Uganda na Simba SC ya Tanzania.

Nafasi ya pili katika Kundi hilo inashikwa na Horoya AC ya Guinea iliyojizolea alama nne baada ya kucheza michezo miwili, huku Vipers SC ikiambulia alama moja na Simba SC ikiburuza mkia kwa kushindwa kuokota alama yoyote hadi sasa.

Polisi yateta na wafugaji vibali uuzaji wa mifugo
Simba SC yapangua uzushi mitandaoni