Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema chama chake cha African National Congress (ANC), ni dhaifu kufuatia hasara ya kihistoria iliyotokea katika uchaguzi wa manispaa mwaka 2021.
Kiongozi huyo wa chama kinachotawala Afrika ya Kusini, aliyazungumza hayo katika mazungumzo yanayoendelea ya siku tatu yaliyoanza Julai 29 – 31, 2022 kuzungumzia na kushughulikia tuhuma za ufisadi dhidi ya wanachama wa ANC, huku uchumi wa nchi hiyo ukiendelea kukabiliwa na mizozo ya kijamii.
Wakosoaji wa masuala ya kisiasa wanadai Serikali haina mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na umaskini, ukosefu wa usawa na asilimia 34.5 ya ukosefu wa ajira, unaozidishwa na janga la Uviko-19 ikiwemo huduma za kimsingi kama vile umeme na maji.
Uungwaji mkono kwa ANC, ulipungua chini ya asilimia 50 kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba mwaka jana, huku kukiwa na ukatishwaji wa tamaa na chama hicho ambacho kimetawala nchi hiyo kwa takriban miongo mitatu tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi.
“Chama cha ANC leo kiko katika hali dhaifu na dhaifu zaidi tangu kuja kwa demokrasia,” Ramaphosa aliwaambia wajumbe katika mazungumzo ya kujadili mwelekeo mpya wa chama jijini Johannesburg.
Ramaphosa alisema, “Udhaifu huu unadhihirika katika kutoaminiwa, kukatishwa tamaa, kukatishwa tamaa kunakoonyeshwa na watu wengi kuelekea harakati zetu na Serikali yetu, na tutaangalia ripoti ya uchunguzi wa ufisadi wa serikali iliyochapishwa mapema mwaka huu ikitaja zaidi ya wanachama 200, wakiwemo baadhi ya maafisa wakuu.”
Amesema, chama cha Kiongozi aliyekuwa akipinga ubaguzi wa rangi Nelson Mandela sasa kimekuwa na vuguvugu la mgawanyiko unaoashiria mipasuko ambayo inaendeshwa na ushindani wa vyeo na upatikanaji wa rasilimali za umma, sambamba na mambo ya upendeleo.
Mazungumzo hayo, ni utangulizi wa kongamano la kitaifa la uchaguzi la ANC mwezi la Desemba, wakati chama hicho kitakapofanya uchaguzi wa ndani kumchagua mgombea kwa uchaguzi ujao wa urais.
Ramaphosa anatarajiwa kuwania muhula wa pili wa miaka mitano, lakini huenda akakabiliwa na changamoto kutoka kwa mrengo wa chama ambacho ni mtiifu kwa rais wa zamani Jacob Zuma, ambaye amekuwa akituhumiwa kwa ufisadi.
Chama hicho pia kinakabiliwa na matatizo ya kifedha, kikiwa kimetatizika kulipa mishahara katika miezi ya hivi karibuni, huku makumi ya wafanyikazi wa chama walivamia nje ya ukumbi wa mkutano, wakipinga kutolipwa mishahara yao ambapo Ramaphosa mwenyewe amekumbwa na kashfa kufuatia uvamizi wa shamba lake la wanyama pori na mifugo.