Ligi ya mpira wa kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) inatarajiwa kuanza Mei 6, mwaka huu ikishirikisha timu 13 za wanaume na 12 za wanawake.
Mkurugenzi wa Kamisheni ya Mipango, Maendeleo na Masoko wa Chama cha Kikapu Dar es Salaam, Terence Mhumbira amesema wanatarajia kuwa na timu zaidi hapo baadaye za wanawake ili kuweka usawa.
Amesema jina la ligi kwa sasa litabadilika kutoka RBA hadi BDL akisema wameangalia sababu za kibiashara huku akieleza kuna timu mbili za wanawake zimeongezeka msimu huu kuonesha wazi kutakuwa na ushindani mkubwa.
“Tuko kwenye maandalizi ya ligi Mkoa wa Dar es Salaam tukitarajia itakuwa ya kiwango cha juu kutokana na timu zilizopo, washiriki wanatakiwa waanze maandalizi ili kuleta ushindani na mwisho wa siku kupata wawakilishi bora wa kushiriki ligi ya taifa,” amesema.
Timu za wanawake zitakazoshiriki ni DB Lioness, JKT Stars, Jeshi Stars, Kurasini Dibas, Mchenga Queens, Pazi Queens, Ukonga Queens, Vijana Queens, UDSM Queens, Polisi Queens, Oilers Princess na Magereza.
Kwa upande wa timu za wanaume kuna ABC, Chui, Dar City, DB Oratory, JKT, Jogoo, Mchenga, Mgulani, Oilers, Pazi, Polisi, Savio, UDSM Outsiders, Ukonga Kings, Ukonga Warriors na Vijana City Bulls.