Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amewataka wataalamu wa afya kuwa na mikakati ya pamoja itakayorahisisha kupunguza vifo vya mama na mtoto ,kwani katika takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa kulikuwa na vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kwa mwaka 2020 vilikuwa 1,640 na mwaka 2021 vilikuwa 1,588.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wataalam wa Afya kanda ya Kaskazini kinacholenga kujadili namna ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga .
“Lengo la Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha vifo vya mama na watoto havitokei hivyo ni muhimu ninyi kama madaktari na wataalam wa afya kuwa vifo vinapungua au kuisha kabisa”amesema.
Aidha,Mkuu huyo wa Mkoa wa Kilimanjaro amefafanua kuwa takwimu za watoto waliozaliwa wafu ni 17339 kwa mwaka 2019, huku kanda ya Kaskazini ilikuwa 150 mwaka 2020, vifo 175 mwaka 2019 na vifo 135 mwaka 2022.
Naye, Afisa Programu Wizara ya Afya,Idara ya Afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto Jackline Ndanshau amesema wao kama wataalam wa Afya wataendelea kuhakikisha wanatoa mafunzo kikanda huku mratibu wa Afya ya Uzazi,Mama na Mtoto Kanda ya Kaskazini Haikamesia Malisa akisema wataendelea kutoa huduma za afya kwa ueledi ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Hali ya vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kwa ngazi ya mikoa, vilikua mkuu huyo wa mkoa amesema ; mkoa wa Kilimanjaro; mwaka 2020 vifo 51, mwaka 2021 vifo 66 na mwaka 2022 vifo 39 huku Mkoa wa Arusha; mwaka 2020 vifo 46, mwaka 2021 vifo 55 na mwaka 2022 vifo 61 na mkoa wa Tanga; mwaka 2020 vifo 53, mwaka 2021 vifo 55 na mwaka 2022 vifo 35.
Takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa vifo vya watoto wachanga kwa mwaka 2021 vilikuwa 6,720. Idadi ya vifo vya watoto wachanga kwa kanda ya Kaskazini vilikuwa 1,229 mwaka 2019, vifo 1,015 mwaka 2020, mwaka 2021 vifo 1,189 na mwaka 2022 vifo 1,059.