Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amewataka Maafisa Kilimo wote kujipima na kuona kama kweli wanaendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano inayowataka kutoka ofisini kuwafuata wakulima na kuhakikisha kero mbalimbali zinazowakabili zinasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.
Ameyasema hayo katika ziara yake mkoani humo ambapo alitembelea Tarafa ya Mazombe ambako amezindua miradi ya maendeleo na kufanya mkutano wa kuzungumza na wananchi katika eneo la Mji mdogo wa Ilula.
Amesema kuwa hafurahishwi na tabia ya baadhi ya maafisa wa serikali wakiwemo wale wenye dhamana ya kusimamia kilimo kugeuka kuwa watu wa ofisini na hawatoki kuwafuata wakulima kujua changamoto zao na kuzitatua.
Aidha, Hapi amewataka watendaji wa halmashauri kuchapa kazi kwa malengo ili kuiepusha serikali na lawama ambazo kimsingi wao wanalipwa mishahara kuzitatua.
Katika Mkutano huo maarufu kama ‘Mahakama ya Wananchi’, kila mkuu wa idara husika ya halmashauri aliwajibika kusimama na kutolea ufafanuzi kero zilizoulizwa na wananchi katika idara yake.
Hata hivyo, kuhusu shida ya Maji, RC Hapi amewatoa Shaka wananchi wa Ilula kuwa Serikali ya CCM imeshatenga fedha za mradi wa maji Ilula kiasi cha bilioni 4.9 ambazo zitajenga mradi wa maji, kazi ambayo imeshaanza na inatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka 2019. Mradi huo ambao ameutembelea, utatatua kero ya Maji katika mji wa Ilula kwa kutoa usambazaji wa sasa wa 47% na kufikisha zaidi ya 87%.