Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amesema si watu wote wanaofariki na kuzikwa mkoani humo vifo vyao vinatokana na UVIKO-19, bali pia hutokana na matatizo mengine ikiwemo saratani na umri mkubwa.
Kagaigai ameyasema hayo wakati akizindua zoezi la chanjo na kuongeza kuwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro ni watafutaji katika mikoa mingine na desturi yao unapofariki lazima uzikwe nyumbani.
“Si wote wanaozikwa hapa mkoani Kilimanjaro wamefia hapa, ni kwamba wanasafirishwa kuletwa hapa kutoka maeneo mengine na ndio mana kunakuwa na misiba mingi na siyo misiba yote inatokana na UVIKO-19,” Amesema Kagaigai.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoani humo, Patrick Boisafi amesema iko haja kwa Wanakilimanjaro kujitafakari upya katika suala la kuzika nyumbani pindi ndugu anapofariki nje ya mkoa huo, ikiwezekana wazike huko huko au waende wachache katika mazishi.
Boisafi amesema kumekuwa na maneno mengi kwenye mitandao ya kijamii ya kwamba Kilimanjaro inaongoza kwa watu wengi kufariki lakini ikumbukwe ni utamaduni wa Wachaga kuzika kwao pindi mtu anapofariki.
Mkoa wa Kilimanjaro una vituo 22 vya kutolea chanjo dhidi ya UVIKO-19, ambapo tayari wananchi zaidi ya 10,000 wameshachanjwa hadi kufikia Agosti 07, 2021.