Serikali mkoani Kagera imejipanga kuhakikisha ifikapo tarehe 30 mwezi wa Sita mwaka huu kaya zote mkoani humo zinakuwa na vyoo bora na kuvitumia na kuziagiza taasisi zote za umma kuhakikisha zinakuwa na vyoo bora.

Mkoa wa Kagera unatarajia kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Usinichukulie Poa Nyumba ni Choo’ siku ya jumamosi  tarehe 25 mwezi huu kikanda katika yenye lengo la kuhamasisha kujenga na kutumia Vyoo bora.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa mkoa Kagera, Bregadia Jenerali Marco Gaguti amesema kuwa mkoa kwa kushirikiana na mamlaka husika umeendelea kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora ngazi ya kaya na taasisi kupitia uhamasishaji wa jamii.

Amesema kuwa kuanzia mwaka 2012 kampeini hiyo ilipoanza asilimia 35 ya kaya mkoani kagera hazikuwa na choo ambapo vyoo bora ilikuwa asilimia 20 tu lakini sasa kwa jitihada za mkoa kaya zisizo na vyoo imepungua kutoka asilimia 35 hadi asilimia 5  huku vyoo bora vikiongezeka kutoka asilimia 20 hadi asilimia 55.

“Kampeni hii haitakuwa na maana endapo baadhi ya tabia mbaya zikiachwa kushamiri, nyote mnaelewa uwepo wa tabia ya kujisaidia hovyo wakati wa safari maarufu kama kuchimba dawa. Kwa bahati nzuri ndani ya mkoa wa wetu kuna vyoo katika maeneo yaliyopo kando ya barabara kuu za Bukoba-Nyakanazi na Bukoba Mtukula, hivyo hakuna kisingizio cha kujisaidia porini.”amesema Gaguti.

Aidha, mkuu wa mkoa Kagera ameongeza kuwa kampeni hiyo itakayokuwa inaendeshwa na msanii, Mrisho Mpoto itazunguka halmashauri zote za mkoa wa Kagera na kuwataka wakuu wa wilaya zote na wakurugenzi kuweka matamshi kwa maandishi kuhusu ni lini kula wilaya itatekeleza agizo hili.

Kwaupande wake mratibu wa kampeni ya taifa ya usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima amesema kuwa namna wizara ilivyojipanga kuhakikisha kila kaya nchini inakuwa na choo bora na kukitumia ili kuweza kuthibiti uwepo wa magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza endapo jamii haitakuwa na vyoo bora.

 

Vyombo vya habari vyatakiwa kutoa habari zenye ukweli
Kafulila autaka mpango kazi wa kisheria kukamilika mapema