Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenarali Marco Gaguti ameiagiza halmashauri ya wilaya Biharamulo mkoani humo kuhakikisha inawachukulia hatua watumishi waliohusika na ubadhilifu wa fedha za umma katika halmashauri hiyo na kutoa siku mbili kurejeshwa kwa fedha ambazo zimetumika kinyume na malengo.
Ametoa maagizo hayo katika hotuba yake iliyosomwa na mkuu wa wilaya Biharamulo kwenye kikao maalumu cha kujibu hoja za CAG ambapo jumla ya hoja 81 ziliibuliwa na CAG zikiwemo matumizi mabaya ya fedha za umma pamoja na kukua kwa deni la halmashauri hiyo.
Amesema kuwa ripoti ya CAG inaonyesha kuwa fedha nyingi katika halmashauri hiyo zinatumika na vielelezo havionekani na kuongeza kuwa halmashauri hiyo ina miradi viporo isiyokamilika ikiwemo ujenzi usioridhisha wa maabara katika baadhi ya shule za sekondari.
Kufuatia hali hiyo mkuu wa mkoa amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kusimamisha mishahara ya watumishi wote ambao wanakusanya mapato ya ndani kwa kutumia mashine hadi pale watakapolipa pesa wananzodaiwa, na kutoa siku 14 kwa kila anayedaiwa mapato wawe wamelipa.
Kwa upande wao madiwani wa halmashauri hiyo wamesema kuwa hoja za CAG zinatakiwa kufanyiwa kazi ili kuweza kuwaletea wananchi wa Biharamulo maendeleo na kumuomba mkurugenzi kutekeleza maagizo ya mkuu wa mkoa kwa kuhakikisha wale wote waliohusika wanashughulikiwa kikamilifu.
Aidha, mkuu wa wilaya hiyo, Saada Malunde ameitaka halmashauri hiyo kuzingatia sheria za matumizi ya fedha ili kuweza kuepuka hoja za CAG zinazoweza kujitokeza.
“Nimekuwa nikipiga mahesabu hapa kwamba fedha zote zirejeshwe wakati zimeshatumika, tunaweza kutumia pesa zote za mapato yote ya ndani hatutaweza kuzilipa, ninachoomba tujihadhali na matumizi ya fedha yasiyofuata kanuni na taratibu.” amesema DC Malunde.
Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa kutokana na kuwa na miradi viporo ameelekeza kutokuanzisha miradi mipya hadi pale miradi iliyododa itakapo kamilikia.
-
Manispaa ya Ilala yatakiwa kuharakisha uundwaji wa kamati za walemavu
-
LIVE IKULU: Makabidhiano ya Dhahabu iliyokamatwa nchini Kenya inawasilishwa na Mjumbe wa Rais Kenyatta
-
Kamanda Muroto awatahadharisha matapeli jijini Dodoma