Haruna Juma, Mpanda – Katavi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesikitishwa na baadhi ya Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kujihusisha na uchochezi wa migogoro katika eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji la Luhafwe lenye ukubwa wa hekta 46,000 (ekari 115,000).

Hali hiyo imejitokeza baada ya RC Mrindoko akiambatana na Kamati Ulinzi na Usalama Mkoa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta kufanya ziara ya kutembelea eneo hilo na kukutana na taarifa ya eneo moja kumilikishwa kwa wawekezaji zaidi ya mmoja.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amemwambia RC Mrindoko kuwa katika eneo hilo, Halmashauri imepokea fedha kutoka kwa kampuni mbili ambazo ni Seedland na Meru Agro kitendo ambacho kinaleta ugumu kwa eneo hilo kuendelezwa.

Kufuatia hatua hiyo, RC Mrindoko amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Shaban Juma kufika ofisini kwake Novemba 20, 2023 akiwa na nyaraka zinazoonesha ramani ya eneo la Luhafwe na mikataba yote ya uwekezaji waliyoingia na wawekezaji ikiwemo kiasi cha fedha halmashauri ilizolipwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa mbele ya RC Mrindoko imeeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Septemba 2023 imefanya shughuli ya upimaji na mpaka sasa wawekezaji wakubwa waliotajwa kupewa mashamba ni MPM (Mufindi Paper Mills), Seed Land, Mero Agro na ASA.

Eneo la uwekezaji la Luhafwe lililotangazwa mwaka 2018 lina jumla ya mashamba 116 ambapo kati ya hayo mashamba 13 yana ukubwa wa ekari 2000-5000, mashamba 17 yana ukubwa ekari 500, mashamba 5 yana ukubwa wa kati ya ekari 500-1000 na mashamba mengine 81 yana ukubwa wa chini ya ekari 500-1000.

Jengo la kujifungulia Dumbeta kuwapunguzia adha Wananchi
Suluhisho changamoto ya Jangwani lapatikana