Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu, Zelote Stephen ameishauri kamati ya maandalizi ya nanenane nyanda za juu kusini kufikiria kushirikisha nchi za SADC ili kuongeza hamasa na kuleta ushindani kwa watanzania wafahamu yanayofanyika katika nchi za jirani.
Ameyasema hayo wakati wa majumuisho mara baada ya kutembelea mabanda 16 ya bidhaa mbalimbali za kilimo katika maonesho ya nane nane kwa kanda ya nyanda za juu kusini yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
“Tuachane na mazoea, maonyesho haya yana miaka 25 sasa tuyaboreshe zaidi, isiswe ni mikoa hii tu saba, tupanue wigo, kwakuwa huku ni nyanda za juu kusini basi tufikirie kuzishirikisha nchi za SADC ambazo zitasaidia kubadilishana biashara na teknolojia pamoja na kutafuta masoko,” Amesema Zelote.
Amesema kuwa nchi ya Tanzania inafikika kwa njia zote, ardhini, majini na angani huku akitaja meli mbili zilizozinduliwa Mkoani Mbeya na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, treni ya TAZARA pamoja na ndege zinazomilikiwa na shirika la ndege Tanzania.
Aidha amezishauri halmashauri kuanza maandalizi kwa kuwa na siku maalum kwaajili ya maadhimisho hayo kihalmashauri ili kuwapa ujuzi na kujua ubora wa vitu ambavyo vinaweza kupelekwa kwenye maadhimisho ya nane nane kikanda ili kuimarisha ushindani na kumpa kila mwananchi nafasi ya kuelimika ili kuwa na kilimo chenye tija.
Hata hivyo, Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, kwa pamoja wamewataka wahusika kutoa elimu kwa wakulima wa hali ya chini ili waweze kupata matokeo chanya ya maonyesho hayo.