Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule leo tarehe 15/03/2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan, Yasushi Misawa na balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Tri Yogo Jatmiko katika Ofisi yake Dodoma.
Kwa nyakati tofauti Balozi wa Japan, Yasushi Misawa ameonesha nia ya kuhamia katika Jiji la Dodoma kuendeleza juhudi ya Serikali katika kuhakikisha balozi na mashirika ya kimataifa yanahamia Mkoani huo, ambao ni Makao Makuu ya nchi.
Amesema, pia ujio wa Ubalozi wa Japan katika makao makuu ya nchi una lengo la kuimarisha ushirikiano uliopo wa muda mrefu baina ya nchi hizi mbiliikiwa ni pamoja na kuona maeneo mahsusi ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo na ujenzi wa viwanda.
Naye Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Tri Yogo Jatmiko amesema ujio wake umelenga kuanzisha ushirikiano baina Jiji la Dodoma na Jiji la Jakarta na kuongeza kuwa Indonesia iko tayari kushirikiana na Jiji la Dodoma katika kuendelea maeneo ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vya kukamua mafuta kupitia miti ya Muarobaini.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema Serikali imefanya maboresho makubwa katika Mkoa wa Dodoma, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na huduma za afya huku viwanja 67 vimetengwa katika mji wa Serikali Mtumba kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Serikali na mashirika ya kimataifa.
Amesema, “Tunawakaribisha Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu, Fahari ya watanzania, Serikali imeimarisha kila sekta na baadhi ya Balozi na mashirika ya kimataifa yamehamia,nitoe shime kwao kufungua ofisi hapa na kuendelea kushirikiana nasi katika masuala ya maendeleo ya nchi yetu.”