Mabingwa wa kihistoria katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, Real Madrid kesho wataanza kampeni ya kuwania ubingwa wa michuano hiyo kwa kucheza dhidi ya mabingwa wa soka nchini Ufaransa, Paris St. Germain katika mchezo wa kundi A.
Tayari Real Madrid wameshawasili jijini Paris kwa ajili ya mchezo huo ambao utaunguruma kwenye uwanja wa Parc des Princes wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 47,929 walioketi.
Baada ya kuwasili jijini humo wakitokea Madrid-Hispania, ilibainika beki wa kushoto kutoka Brazil Marcelo Vieira da Silva Júnior, hayupo kikosini, na ndipo wa mji wa Paris walipohoji kulikoni mtu huyo hakuongozana na kikosi?
Hata hivyo baadae taarifa za kutokuwepo kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 31, zilichapishwa kwenye Tovuti ya klabu, zikieleza kuwa Marcelo hakusafiri na kikosi, kutokana na majeraha ya mgogongo yanayomsumbua kwa sasa.
“Baada ya kufanyiwa vipimo, ilibainika Marcelo hatoweza kucheza mchezo wetu dhidi ya PSG, daktari wa timu ameshauri abaki ili aendelee na matibabu,” ilieleza taarifa hiyo.
Beki wa kushoto kutoka Ufaransa Ferland Sinna Mendy aliyesajiliwa wakati wa majira ya kiangazi akitokea Olympic Lyon ya Ufaransa kwa Euro million 53, anatarajiwa kuziba nafasi ya Marcelo katika mchezo wa kesho.
Real Madrid pia itawakosa baadhi ya wachezaji wake kama Isco, Luka Modric, Marco Asensio na Fede Valverde wanaoendelea kuuguza majeraha, huku Sergio Ramos na Nacho Fernandez wakitumikia adhabu.