Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limempanga Issa Sy kutoka Senegal kuwa mwamuzi wa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba SC dhidi ya Mabingwa watetezi Wydad Casablanca utakayochezwa Jumamosi (April 22) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Takwimu za michezo 15 iliyopita ya michuano ya klabu Barani Afrika ambayo amechezesha mwamuzi huyo, zinaweza kuipunguzia Presha Simba SC kwani amekuwa na historia ya bahati kwa timu mwenyeji ambapo mara nyingi akichezesha zimekuwa zikipata ushindi huku mara chache zikipoteza.
Katika michezo15 ya mashindano ambayo iliyochezeshwa na Sy awali, timu mwenyeji zilishinda mara tisa, sare mbili na zilipoteza nne.
Ni mwamuzi ambaye Simba SC wanapaswa kuwa makini naye hasa katika suala la nidhamu kwani amekuwa na hulka ya kumwaga kadi na kuthibitisha hilo, katika michezo 15 iliyopita alitoa kadi 70 sawa na wastani wa kadi 4.5 kwa kila mchezo, kadi za njano 67 na kadi nyekundu tatu.
Katika mchezo huo, Sy atasaidiwa na Bangoura Nouha (Senegal), Desire Ngoh wa Ivory na mwamuzi wa akiba ni Msenegal mwenzake, Maguette Ndiaye.
Kama ilivyo utaratibu wa CAF wa kutumia Teknolojia ya usaidizi wa video kwa waamuzi (VAR) kuanzia hatua ya Robo Fainali hadi Fainali, tayari wataalaam wa ufungaji wa teknolojia hiyo wapo nchini na leo asubuhi, waamuzi wawili wa VAR ambao watamsadia Sy walitarajiwa kuwasili nchini kwa mujibu wa meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.
“Mechi yetu na Wydad itakuwa na VAR. Maofisa wake watafika leo na Wydad wao watafika leo saa 5 asu-buhi wakiwa na msafara wa watu 50 huku waamuzi na wao watafika nchini leo. Kikubwa mashabiki zetu ni kuja uwanjani ili upate burudani,” alisema Ahmed Ally