Mchezo wa Kwanza wa Kundi B Kombe la Shirikisho kati ya US Monastir (Tunisia) dhidi ya Young Africans (Tanzania) utachezeshwa na mwamuzi kutoka Benin. Djindo Louis Houngnandande.
Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 37, ana historia ya kumwaga kadi kwa wachezaji wanaofanya makosa, hivyo wachezaji wa US Monastir (Tunisia) na Young Africans (Tanzania), wanapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa michezo 14 ya kimataifa ngazi ya vilabu ambayo Mwamuzi Djindo alichezesha, ametoa kadi 52 ambazo 51 ni za njano na moja nyekundu, ikiwa ni wastani wa kadi 3.7 kwa mchezo.
Hata hivyo Mwamuzi huyo amekua kama na bahati mbaya, kwani kwa asilimia 99 kila anapocheza michezo ya kimataifa, timu inayokua ugenini hupoteza, lakini hiyo haizuii Young Africans kupambana na kupata ushindi ugenini.
Kuanzia Desemba 8, 2019 alipoanza kuchezesha mashindano ya Kimataifa ya CAF, ni timu moja tu ilipata ushindi ugenini ambayo ni Jaraaf ya Senegal ikishinda 1-0 dhidi ya Salitas ya Burkina Faso, Aprili 12, 2021.
Young Africans itacheza dhidi ya US Monastir ya Tunisia Jumapili (Februari 12), katika Uwanja wa Hammadi Agrebi, mjini Tunis.