Mshambuliaji kutoka Brazil na Klabu ya Tottenham Hotspur, Richarlison de Andrade ‘Richarlison’, amesema kocha wa zamani wa klabu hiyo, Antonio Conte, alimfokea kwa takriban saa mbili katika mkutano wa timu.
Mchezaji huyo alivumilia msimu ngumu wa kwanza katika Klabu ya Spurs msimu uliopita chini ya Conte kabla ya Muitaliano huyo kutimuliwa na Uongozi mwezi Machi mwaka huu.
Richarlison alikuwa amemkosoa Conte kufuatia kuondolewa kwa Tottenham kutoka hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya timu hiyo kujibu na kumweleza mchezaji huyo kuwa “mbinafsi.”
Richarlison alisema alikosea kumkosoa kocha wake hadharani na akapokea adhabu yake mbele ya wachezaji wenzake.
“Ni kweli nilijifanya mjinga kwa kusema kwenye mahojiano kwamba nahitaji muda na kila kitu kingine, ilikuwa baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini nilimwomba msamaha,” amesema Richarlison.
Conte alimsajili Richarlison kutoka Everton mwanzoni mwa msimu wa 2022-23, lakini mshambuliaji huyo alikuwa na wakati mgumu kutokana na majeraha.