Ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa (UN) imeeleza kuwa huenda Korea Kaskazini imezalisha kombora jipya la kinyuklia lenye umbo dogo zaidi lakini linaweza kutoa madhara yanayoendana na makombora mazito.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na watalaam UN wanaosimamia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini imebainisha kuwa inaaminika Korea Kaskazini ilifanikiwa katika majaribio sita ya nyuklia ambayo yaliisaidia kutengeneza makombora hayo yenye umbo dogo.
Imeelezwa kuwa aina hiyo mpya ya makombora itaisaidia nchi hiyo kuendana zaidi na mabadiliko ya kiteknolojia na kuyafanya yabebeke kirahisi.
Waziri Kairuki atembelea maonesho ya Nanenane, akumbusha zabuni kwa makundi maalum
Kwa mujibu wa Reuters ambao wameeleza kuiona ripoti hiyo, imewasilishwa kwenye Kamati ya wajumbe 15 ya Baraza la Umoja wa Mataifa, jana, Agosti 3, 2020.
“Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea inaendelea na program yake ya makombora ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na kuzalisha silaha kwa kutumia uranium zenye uwezo mkubwa zaidi,” Reuters wameikariri ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja tu tangu Kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong-un atangaze kuwa hakutakuwa na vita tena kwani makombora ya nyuklia ya nchi hiyo ni kwa ajili ya kujilinda na kuhakikisha usalama wake, ingawa kuna shinikizo kubwa kutoka nje.
Umoja wa Mataifa uliiwekea Korea Kaskazini vikwazo vya kiuchumi tangu mwaka 2006 kutokana na program yake ya makombora ya nyuklia. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia liliongeza vikwazo kuhakikisha haipati msaada wa kuendeleza program hiyo.
Aidha, nchi hiyo ilisitisha majaribio ya makombora ya kinyuklia tangu Septemba, 2017, na kwa mara ya kwanza Rais wa Marekani, Donald Trump alikutana na Kim Jong-un na wakafanya mazungumzo mara tatu kwa nyakati tofauti.