Ingawa vyakula hutofautiana kati ya jamii moja na nyingine, mkate unaweza kuwa moja kati ya vyakula ambavyo hupatikana na kutumiwa na jamii karibu zote duniani kote. Lakini chakula hiki kimebainika kuwa na uwezo wa kusababisha saratani kupitia mtambo wa kuoka au kuchoma.
Kwa mujibu wa Wakala wa Viwango vya Ubora vya Vyakula Uingereza (FSA), mkate unaookwa hadi kufikia hatua ya kubadili rangi kuwa ya hudhurungi au kahawia huwa na uwezo mkubwa wa kusababisha saratani kwa mlaji.
Wataalamu wameongeza kuwa sio mkate pekee, chips na viazi pamoja na vyakula vingine pia havifai kuchomwa au kupikwa hadi kupata rangi ya hudhurungi. Wameeleza kuwa vyakula hivyo vinapaswa kupikwa hadi kuwa na rangi ya manjano iliyokolea dhahabu na sio vinginevyo.
Wakieleza sababu za kusababisha saratani, wataalam hao wamesema kuwa vyakula vyenye ‘wanga’ au kukaangwa kwa muda mrefu katika kiwango cha juu sana cha joto hutengeneza kemikali ya ‘Acrylamide’ ambayo inaweza kusababisha saratani.
Imeelezwa kuwa vyakula vyenye kiwango cha juu cha wanga hasa vinavyopikwa viwandani kwa zaidi ya nyuzi joto 120 kama kaukau, mkate, biskuti, keki na kahawa vinauwezekano mkubwa wa kutengeneza ‘Acrylamide’.