Kashobi Shida mwenye umri wa miaka ishirini na sita, mtoto wa dereva wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa huo baada ya kupata ajali ya gari amefariki dunia.
Kasobi alilazwa hospitalini hapo Jumapili, Agosti 4,2019 baada ya kupata ajali wakati akiendesha gari linalotumiwa na baba yake Shida Masaba (55) kumuendesha Mkuu wa mkoa wa Mara.
Hata hivyo, ajali hiyo iliyosababisha baba mzazi wa Kashobi kulazwa katika hospitali ya mkoa huo kutokana na kushidwa kupumua vizuri. Madaktari walisema anasumbuliwa na shinikizo la damu .
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya mkoa wa Mara Dkt. Hosea Bisanda amethibitisha kutokea kwa kifo hicho usiku wa kuamkia leo.
Dkt Bisanda ameeleza kuwa Kasobi alipokelewa hospitalini hapo Augosti 4, 2019 huku akiwa na maumivu sehemu za tumbo, kifuani na mchubuko kwenye kiwiko cha mkono wake wa kulia.
Amesema kuwa baada ya kupokelewa Kasobi alipewa matibabu na kwamba hadi jana asubuhi hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.
”Mchana hali yake ilibadilika na hivyo jopo la madaktari wa upasuaji wakaamuamua akafanyiwe upasuaji ambao ulifanyika vizuri lakini ghafla tena hali ikabadilika baada ya upasuaji na akafariki dunia usiku wa jana saa 2,” Dkt. Bisanda anakaririwa.