Milio ya risasi imesikika usiku kucha karibu na ikulu ya Guinea-Bissa baada ya Wanajeshi kumwachilia huru Waziri wa Chama Kikuu cha Upinzani, aliyekuwa amekamatwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Milio hiyo ya risasi ilisikika kwa mara ya kwanza majira ya usiku takriban kilomita mbili kutoka Ikulu ya Rais wa Taifa hilo huku majibizano ya risasi yaliendelea kusikika pia baada ya saa sita usiku katika kitongoji cha Antula, kilichopo nje kidogo ya mji mkuu wa Bissau, eneo analoishi Jenerali wa Jeshi.
Milio ya risasi pia iliendelea Ijumaa asubuhi ya Desemba Mosi, 2023 huku magari ya kijeshi yakizunguka barabarani huku wakaazi wakielekea kazini na mashuleni.
Kufuatia tukio hilo, Afisa msaidizi wa mawasiliano ya Ikulu ya Nchi hiyo amesema Ofisi ya rais haina uhusiano wowote na tukio hilo na kwamba hakuna maoni yoyote kwa niaba yao kuhusu kinachoendelea.