Imefahamika kuwa, kiungo mshambuliaji kutoka nchini Algeria na klabu ya Leicester City Riyad Mahrez, alithitaji kujiunga na vinara wa ligi ya England Manchester United, katika siku ya mwisho ya usajili wa majira ya kiangazi.
Mahrez aliyeripotiwa kuhaha siku ya mwisho ya usajili, baada ya kuondoka kwenye kambi ya timu yake ya taifa iliyokua inajiandaa na michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia ukanda wa Afrika, amebainika alihitaji sana uhamisho wa kujiunga na kikosi cha Jose Mourinho lakini ilishindikana.
Wakati siri hiyo ikifichuliwa na vyombo vya habari vya England, taarifa zilizoripotiwa siku ya mwisho kabla ya dirisha la usajili kufungwa zilieleza kwamba, kiungo huyo alikua anawaniwa na klabu za Arsenal, Chelsea, FC Barcelona na AS Roma.
Vyombo vya habari vya England vimeeleza kuwa, kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa Mahrez kujiunga na moja ya klabu hizo, lakini alionyesha kusita kwa kuamini huenda mipango yake ya kusajiliwa na Man Utd ingefanikiwa dakika za mwisho.
Kushindikana kwa mipango hiyo kumefanya Mahrez kuendelea kubaki Leicester City licha ya kuwahi kueleza kuwa, hapendezwi na maisha ya klabu hiyo, tangu iliposhindwa kutetea ubingwa wa England msimu uliopita.