Kocha Mkuu wa Simba SC, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amewahakikishia mashabiki kwamba kuna mapinduzi makubwa yanakuja kwenye usajili wa klabu hiyo.
Robertinho amesema kuwa ameshakutana na mabosi wa juu wa klabu na kutengeneza mikakati ya kukisuka kikosi chao na ameridhika na makubaliano kwamba mastaa wapya watakuja kuwarudishia hadhi iliyopotea kwenye mataji.
“Kitu ambacho kipo mbele yetu sasa ni kumalizia hizi mechi mbili za mwisho za ligi. Mimi ni kocha ninayetaka kushinda kila wakati na hiki ndicho pia mashabiki wa Simba wanastahili,” alisema kocha huyo ambaye kwa uchache anataka wachezaji 10 wapya.
“Tutakapomaliza msimu wapo wachezaji tutaachana nao kwa heshima lakini (kupitia) vikao vyangu na viongozi wa klabu tutakwenda kuleta wachezaji bora ambao watarudisha heshima ili tuwe kwenye eneo ambalo tunastahili,” amesema
“Tutaleta wachezaji ambao wana njaa ya mafanikio kwa hadhi ya Simba SC na sio vinginevyo. Simba SC ni klabu ya makombe sio kuwa hapa tulipo,” alisema kocha huyo ambaye inafahamika ameshamalizana na Moses Phiri na atasalia Msimbazi kukiwasha msimu ujao.
Ni msimu wa pili Simba SC imekosa mataji ambayo yamekuwa yakitua kwa watani wao, Young Africans waliopo kwenye ubora na sasa Robertinho amewatumia salamu Jangwani kuna mziki unakuja.
Amewataka mashabiki wa Simba SC watulie wakati huu wanakwenda kumalizia mechi mbili za mwisho za ligi kisha kazi ya kushusha vifaa itaanza na wamejipanga tofauti na misimu iliyopita kwani watafanya kitaalamu zaidi kwa vile levo waliyofikia ni kubwa kwa sasa.
Raia huyo wa Brazil aliongeza kuwa ameachana na ofa nyingi kutoka maeneo mbalimbali baada ya kuridhika na malengo ya Simba kwa msimu ujao hasa kimataifa na uongozi umemtaka atulie.
“Ilikuwa presha kubwa kwangu. Ofa zilikuwa nyingi lakini nimeamua kubaki hapa nawapenda mashabiki wa Simba SC, ila hata viongozi wamekuwa wakinipa ushirikiano mkubwa. Nafurahia mpango mzuri kuelekea msimu ujao,” amesema kocha huyo ambaye amepania kila nafasi msimu ujao iwe na vifaa viwili bandika bandua kama ilivyo kwa watani zao
Taarifa zinaeleza kuwa Augustine Okra, Nelson Okwa, Ismael Sawadogo na Gadiel Michael ni wachezaji ambao kwa kuanzia watang’oka Msimbazi na muda wowote watapewa barua zao.