Kocha Mkuu wa Simba SC Oliviera Roberto ‘Robertinho’ amesema mchezo wa leo Jumamosi (Machi 18) una umuhimu mkubwa sana kwani wanahitaji alama tatu muhimu kwa namna yoyote dhidi ya Horoya AC ya Guinea.
Timu hizo zitavaana katika mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika leo Jumamosi (Machi 18) kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Kocha Robertinho amesema maandalizi ya kuchukua alama tatu za Horoya AC yamekamilika kwa asilimia mia moja huku akiwaachia jukumu la ushindi wachezaji wake.
Robertinho amesema tayari amewaambia wachezaji wake umuhimu wa mchezo huo ambao wanahitaji ushindi ili wapate nafasi ya kufuzu Robo Fainali ya michuano hiyo mikubwa Barani Afrika.
Ameongeza kuwa amepanga kuingia katika mchezo huo kwa kushambulia kwa tahadhari huku wakijilinda kwa dakika zote 90 na sio kujilinda pekee ili kufanikisha malengo yao.
“Niliwaona Horoya AC katika mchezo uliopita nyumbani kwao, ni timu yenye wachezaji wanaocheza kwa kutumia nguvu nyingi na kushambulia ndani ya wakati mmoja.”
“Hivyo tayari nimefanyia maboresho ya kikosi changu katika baadhi ya sehemu ili kuhakikisha tunapata ushindi hapa nyumbani.”
“Sio mchezo mwepesi kwetu, kwani wapinzani wetu wanazitaka pointi tatu zitakazowaweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi,” amesema Robertinho.
Msimamo wa Kundi C hadi sasa Raja Casablanca (Morocco) imeshakata tiketi ya kucheza Robo Fainali ikiwa na alama 12, ikifuatiwa na Simba SC (Tanzania) yenye alama 06, huku Horoya AC (Guinea) ikiwa nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 04 na Vipers SC (Uganda) inaburuza mkia ikiwa na alama 01.