Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amekiri alikuwa na wakati mgumu sana, baada ya kikosi chake kufungwa bao la mapema, dhidi ya Azam FC jana Jumanne (Februari 21).
Simba SC ilikua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, katika mchezo huo wa Mzunguuko wa 23 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliomalizika kwa sare ya 1-1.
Robertinho amesema ni kazi kubwa kwa kocha yoyote duniani anapopata mtihani wa kutanguliwa kwa bao la mapema, hivyo ilimlazimu kufanya mbinu mbadala na kuvuruga mpango aliouandaa kwa ajili ya kuikabili Azam FC.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema pamoja na hali hiyo alipambana kwa kushauriana na Benchi lake la ufundi ili kufanikisha matokeo chanya dhidi ya Azam FC, na hatimaye walipata alama moja.
“Ni mtihani mkubwa kwa Kocha yoyote duniani kufungwa bao la mapema, inaharibu mipango uliojipangia, ndicho kilichotokea katika mchezo huu, tulipambana katika kipindi cha kwanza lakini ilishindikana, kipindi cha pili bado mambo yalikuwa mazito, lakini mwishoni tulipata bao la kusawazisha.”
“Malengo yangu yalikuwa matokeo mazuri ambayo yangetupa alama tatu, lakini haikuwa hivyo tumepata moja, timu yangu imeonesha kupambana, naipongeza Azam FC kwa mchezo mzuri, pia nawapongeza wachezaji wangu.” amesema Robertinho
Sare ya 1-1 inaendelea kuzua Sintofahamu ya Ubingwa kwa Simba SC, ikiwa mbele kwa mchezo mmoja dhidi ya Young Africans, inayoendelea kuongoza msimamo wa Ligi kwa kumiliki alama 59.
Simba SC inaendelea kuwa nafasi ya pili kwa kufikisha alama 54, baada ya kucheza michezo 23, huku Azam FC ikifikisha alama 44 sawa na Singida Big Stars, zote zikicheza michezo 23.