Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameweka wazi kuwa, anataka kuona timu yake inafanya mambo makubwa mawili ambayo ni kuhakikisha wanacheza soka safi na kupata matokeo ya ushindi.
Kauli ya kocha huyo imekuja ikiwa leo Alhamisi (Oktoba 05) Simba SC wanatarajiwa kuwa wageni wa Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa kwenye Dimba la Sokoine, Mbeya.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 7-1, ambapo kwa msimu huu.
Simba SC msimu huu imekuwa na matokeo mazuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kucheza mechi tatu na kushinda zote.
Robertinho amesema anawakumbuka vizuri Prisons kwa sababu waliipa upinzani mkubwa timu yake msimu uliopita, lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanawadhibiti na kuibuka na ushindi.
“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huu, tunategemea kupata upinzani mkubwa. Tunawaheshimu Prisons, tunakumbuka msimu uliopita walitupa mechi ngumu, lakini tumejipanga.
“Tutaingia uwanjani kwa malengo makubwa mawili, moja kucheza soka safi kama ambavyo tumekuwa tukifanya katika ubora wetu, lakini pia lengo la pili ni kushinda,” amesema Robertinho