Baada ya kufuzu Hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kwa sasa anataka kucheza Hatua ya Fainali ya michuano hiyo mikubwa katika ngazi ya Vilabu Barani Afrika.
Simba SC Jumamosi (Machi 18) ilijihakikishia kuwa sehemu ya timu nane zitakazocheza Robo Fainali ya michuano hiyo, baada ya kuwafunga Horoya AC ya nchini Guinea mabao 7-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Simba SC washike nafasi ya pili katika Msimamo wa Kundi C ikiwa na alama 09 huku Raja Casablanca ikiongoza Kundi hilo kwa kuwa na alama 13, zote zikicheza michezo mitano.
Robertinho amesema kwanza kabisa anafuraha kubwa kufuatia kuwa sehemu ya makocha walioifikisha Simba SC Robo Fainali ya michuano ya CAF, na sasa malengo yake anayaelekeza kufikia Hatua ya Fainali.
Robertinho amesema kuwa, hivi sasa anaendelea kukisuka kikosi kitakachokuwa imara na muunganiko mzuri utakaowawezesha kufuzu katika hatua hiyo ya fainali.
Ameongeza kuwa anapata jeuri kutokana na kikosi chake kuimarika zaidi ya kadiri siku zinavyokwenda kwa wachezaji wake kucheza kwa kufauata maelekezo yake na kupata ushindi.
“Kama unakumbuka vizuri, wakati nakabidhiwa niliomba muda wa kutengeneza timu itakayokuwa na muunganiko wa wachezaji watakaokuwa bora.”
“Ninashukuru Mungu hivi sasa kila mmoja anaona mabadiliko yaliyokuwepo ya timu, hivi sasa inacheza soka safi la pasi sambamba na kupata ushindi mzuri.”
“Hiyo inanifanya nifikirie kufika katika hatua ya fainali ya michuano hii mikubwa Afrika, kwani nina amini ubora wa kila mchezaji wangu nitakayempa nafasi ya kucheza,” amesema Robertinho.
Kikosi cha Simba kinaundwa na wachezaji wengi ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kuipeleka timu hiyo Robo Fainali, wakiwemo Clatous Chama, Henock Inonga, Jean Baleke, Aishi Manula, Moses Phiri, Mzamiru Yassin na wengine.