Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema Wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo wa Kesho Jumanne (Februari 21) wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC.
Simba SC itakayokuwa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, itakua na kila sababu ya kulipa kisasi cha kupoteza dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Duru la Kwanza la Ligi Kuu, ambapo bao lililofungwa na Mshambuliaji Prince Dube lilitosha kuizamisha miamba hiyo ya Msimbazi.
Kocha Robertinho amezungumza na Waandishi wa Habari katika Mkutano maalum kuelekea mchezo huo leo Jumatatu (Februari 20), na kueleza mikakati yake ambayo anaamini itakipa ushindi kikosi chake mbele ya Azam FC.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema wanakabiliwa na mazingira magumu ya kucheza michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa wakati mmoja, lakini hawana budi kupambana na kupata matokeo chanya.
“Tuna mchezo mgumu dhidi ya Azam FC kesho, pia tuna mchezo mgumu dhidi ya Vipers SC ya Uganda Jumamosi, kulingana na msimamo ulivyo Kundi C, Wachezaji wangu wanapaswa kupambana kufa na kupona”
“Maandalizi ni mazuri Kuelekea Mchezo wetu dhidi ya Azam FC. Ninafurahi uwepo wa Kanoute na Mkude nadhani nitawatumia kesho” amesema Robertinho
Katika hatua nyingine Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62, alitumia Mkutano na Waandishi wa Habari kuwaomba radhi Mashabiki wa Simba SC kufuatia matokeo mabaya waliyoyapata mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Raja Casablanca.
Amesema Mashabiki wanapaswa kutokukata tamaa na timu yao, na badala yake wanapaswa kuendelea kuwa bega kwa bega ili kufanikisha lengo la kufanya vizuri ndani ya Uwanja.
“Tuna michezo migumu mfululizo, mashabiki nawaomba msikate tamaa kwa sababu mashindano ya nje ni magumu kuliko ya ndani. Mfano Argentina alipoteza mchezo wa kwanza, wachezaji wangekata tamaa wasingekuwa mabingwa Wa Dunia. Tusikate tamaa” amesema Robertinho
Simba SC inakweda Dimbani kesho kuikabili Azam FC ikiwa imejikusanyia alama 53 zinazoiweka nafasi ya pili katika msimamo, huku wapinzani wao kutoka Chamazi wakishika nafasi ya nne kwa kumiliki alama 43.