Kocha Mkuu Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ameweka wazi msimamo wake kwa kuwaambia mabosi wa timu hiyo kuwa katika mapendekezo yake ya usajili anahitaji kuona kila nafasi iwe na zaidi ya wachezaji wawili wenye viwango vya kuzidiana.
Robertinho ametoa kauli hiyo kufuatia Simba SC kukosa makombe yote msimu huu licha ya kuonyesha upinzani mkali mbele ya wapinzani wao Young Africans waliofanikiwa kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo huku wakifanikiwa kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, na Kombe la ASFC.
Robertinho amesema anahitaji kuimarisha kikosi timu yake katika usajili kwa kila nafasi iwe na wachezaji wawili au zaidi wenye ubora na kiwango kizuri.
“Msimu huu tumeshindwa kufikia malengo kwa sababu ya kukosekana kwa nyota wa kikosi cha kwanza kuumia na kushindwa kupata mbadala wao wenye uwiano mzuri na yule tuliyemkosa, tayari nimewasilisha, sasa ni muda wa kuandaa timu nzuri na imara kuhakikisha tunafanya usajili mkubwa kulingana na malengo yetu tuliyojiwekea.
“Nadhani kwa sasa ndiyo jambo la msingi kwa uongozi kuzingatia kulingana na mashindano ambayo yapo mbele yetu kwa sasa na matengenezo ya msimu ujao lazima uongozi uzingatie ubora wa nafasi na aina ya wachezaji kulingana na viwango vyao,” amesema Robertinho