Wakiwa wanajiandaa na mchezo wao wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Young Africans, Kocha Mkuu wa Simba, Robert Olivieira ‘Robertinho’ amechimba mkwara mzito kuwa wametumia uzito wa michezo yao miwili ya AFL, dhidi ya Al Ahly kujiandaa na uzito wa mchezo wa Jumapili (Novemba 05) huku akitenga siku tano sawa na saa 120 kujiandaa na mchezo huo.
Kikosi cha Simba SC kimeshaanza rasmi kambi ya maandalizi ya mchezo huo wa Jumapili (Novemba 05) dhidi ya Young Africans ambapo Mnyama atakuwa mwenyeji mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Simba SC wanaingia katika mchezo huu wakiwa wamecheza mchezo mmoja tu, wa Ligi Kuu Bara baada ya kutoka kwenye ratiba ya mashindano ya African Football League ambayo waliishia Robo Fainali baada ya matokeo ya jumla ya sare ya mabao 3-3.
Robertinho amesema: “Ni kweli tunatarajia mchezo mgumu sana mbele ya Young Africans kutokana na ubora wa kikosi chao, lakini kama kikosi tunajivunia ubora wa maandalizi yetu kuelekea mchezo huu.