Wakati ikijiandaa kuikabili Power Dynamos ya Zambia, katika mechi ya awali ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Barani Áfrika, Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, amesema kikosi chake kitaanza mashindano hayo kwa kishindo.
Simba SC itaanzia ugenini katika mechi ya kuwania kucheza hatua ya makundi katika mechi itakayofanyika kati ya Septemba 15, 16 mwaka huu. Mchezo marudiano utachezwa kati ya Septemba 29, 30 au Oktoba Mosi, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Robertinho amesema pamoja na kikosi kufanya vizuri katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara, nguvu zimeelekezwa katika michuano ya kimataifa.
Kocha huyo raia wa Brazil amesema, wanajua Power Dynamos inaundwa na wachezaji wenye uwezo, hivyo ni lazima aiandae timu yake kutoa upinzani mkali na kushinda mchezo wa ugenini.
Amesema Simba SC itaanza mazoezi ya kujiandaa kuikabili Power Dynamo baada ya mapumziko mafupi na kuweka mikakati kabambe ya kufanikisha ushindi wa mchezo wa ugenini.
“Tunajipanga kuanza michuano ya kimataifa kwa kishindo, lengo ni kufanya vizuri kwa kuvuna alama tatu ugenini, nina imani na kikosi changu,” amesema.
Kocha huyo amesema kwa sasa wachezaji wameanza kuzoeana Uwanjani, kuzoea mazingira, mbinu na anatarajia katika kipindi kifupi kijacho wataanza kutandaza kandanda safi.
Dynamos imefuzu hatua ya pili na kupangwa kucheza na Simba SC baada ya ushindi wa bao 1-0 ikiwa nyumbani katika uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola dhidi dhidi ya African Stars na kupata matokeo ya jumla ya sare ya mabao 2-2.
Awali, timu hiyo ilifungwa mabao 2-1 na African Stars katika mechi ilyopigwa ugenini.
Simba SC itaanza kampeni ya mashindano ya kimataifa ikiwa na rekodi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2003, 2018/19, 2020/21 na 2022/23.
Septemba 6, mwaka huu, Simba SC ilifunga Power Dyanamos ambayo ni Bingwa wa Ligi Kuu ya Zambia kwa mabao 2-0, katika mechi ya kirafiki ya kimataifa katika Tamasha la Simba Day lililofanyika Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Hadi sasa, Simba SC imecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara ikianza kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kuifumua Dodoa jij mabao 2-0.