Aliyewahi kuwa meneja wa klabu bingwa nchini England (Man City) Roberto Mancini, amesaini mkataba wa miaka miwili na shirikisho la soka nchini Italia (FIGC), ambao utamuwezesha kukinoa kikosi cha timu ya taifa hilo.
Kabla ya kufanya maamuzi ya kusiani mkataba wa kukinoa kikosi cha The Azzurri, Mancini mwenye umri wa miaka 53, alilazimika kuvunja mkataba na klabu ya Zenit St Petersburg inayoshiriki ligi kuu ya Urusi, juma lililopita.
Mancini atakua na jukumu la kurejesha heshima ya Italia katika michuano ya kimataifa, baada ya taifa hilo kushindwa kufuzu fainali za kombe la dunia zitakazoanza Juni 14 nchini Urusi.
Jukumu lake la kwanza litakua ni kuiwezesha Italia kufanya vyema katika mchakato wa kuwania ubingwa wa Ulaya katika fainali za 2020, ambazo zitachezwa katika mfumo mpya wa kushirikisha viwanja vya mataifa tofauti barani humo.
Hata hivyo Mancini bado hajatambulishwa katika mkutano na waandishi wa habari, na tayari kituo cha Televisheni cha Sky Italy kimetangaza kocha huyo atatambulishwa kesho Jumanne.
Wakati huo huo hatua ya kusaini mkataba kwa kocha huyo, kunaaminiwa huenda kipenzi chake Mario Balotelli akawa na faraja ya kurejeshwa kwenye kikosi cha Italia, ambacho kitacheza michezo ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Saudi Arabia, Ufaransa na Uholanzi kabla ya kuanza kwa fainali za kombe la dunia.
Balotelli ambaye kwa sasa ana kiwango kizuri akiwa na klabu ya Nice ya Ufaransa, aliokolewa na Mancini miaka kadhaa iliyopita, baada ya kumsajili kwenye kikosi cha Man City.
Tayari mshambuliaji huyo alikua amekosa muelekeo, na baadhi ya mameneja walimgwaya kwa tabia zake za utovu wa nidhamu, lakini Mancini alimini bado ana kila sababu ya kurekebishwa na akacheza soka lake vyema.