Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC wamethibitisha taarifa za kuondoka kwa Kocha Mkuu Roberto Oliveira leo Alhamis (Desemba 29).
Vipres SC imetoa taarifa rasmi ya kuondoka kwa Kocha huyo kutoka nchini Brazil, kupitia Ukurasa wa Instagram, huku wakimtakia kila la kheri katika shughuli zake baada ya kuondoka Klabuni hapo.
Taarifa ya Klabu hiyo iliyochapishwa kwenye Ukurasa wa Instagram inaeleza: Vipers Sports Club inatangaza kwamba Bw. Roberto Oliveira almaarufu Robertinho ameacha jukumu lake kama kocha mkuu.
Klabu inapenda kumshukuru Robertinho kwa juhudi zake za kutochoka kama Kocha Mkuu wakati alipokuwa klabuni hapa na kumtakia mafanikio katika siku zijazo.
Klabu katika muda mfupi itatoa a taarifa kwa Kocha Mpya atakaeongoza Benchi letu la Ufundi kufuatia kuondoka kwa kocha huyo.
Tunabaki Timu Moja Ndoto Moja.
Hata hivyo sababu za Kocha huyo kuondoka Vipers SC hazijaelezwa, zaidi ya kuwepo kwa tetesi huenda akawa amepata kazi mahala kwingine, ambako amepata dili nono zaidi.
Klabu ya Simba SC inahusishwa na mpango wa kumfukuzia Kocha huyo, na mara kadhaa aliwahi kutajwa katika vyombo vya habari, baada ya kuondoka kwa Kocha Zoran Maki mwezi Septemba 2022.
Tayari Uongozi wa Simba SC kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Salim Abdallah ‘Try Again’ amethibisha kuwa, Klabu yao ipo mbioni kumleta Kocha Mkuu mpya, ambaye atasaidizna na Kocha Juma Mgunda ambaye kwa sasa anakaimu nafasi ya Kocha Mkuu.