Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’ ametambulishwa rasmi kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi Simba SC.
‘Robertinho’ ambaye amewahi kufanya kazi katika nchi za Rwanda akiwa na Rayon Sports, Kenya akiwa na Gor Mahia kabla ya kutimkia Uganda akiwana Vipers SC amesaini mkataba wa miaka miwili ambao unaanza kazi rasmi leo Jumanne (Januari 03).
Kabla ya kusaini mkataba huo, Mwenyekiti wa Simba SC Murtanza Mangungu amesema Kocha huyo kutoka nchini Brazil atajiunga na timu visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Mapinduzi inayoendelea kisiwani Unguja.
Amesema wanaamini ujio wa Kocha huyo utaongeza chachu ya ufanisi kazi katika Benchi la Ufundi la Simba SC, ambalo kwa zaidi ya miezi mitatu limekua chini ya Kaimu Kocha Mkuu Juma Ramadhan Mgunda.
“Tunajivunia kuwa na kocha kama huyu mwenye uwezo mkubwa wa kufundisha soka, amekua na mafanikio makubwa katika nchi za Rwanda, Kenya na Uganda,”
“Jukumu kubwa la Simba SC ni kuona Kocha anatufikisha katika malengo tunayoyakusudia na ninaamini hilo linawezekana kutokana na uzoefu alionao kwenye Michuano ya Kimataifa.”
“Pia Kocha huyu ana uzoefu mkubwa wa zile Mechi na wenzetu kwa maana kote alikopita amekua akipata matokeo mazuri, kwa hiyo tunatarajia furaha kutoka kwake tutakapokutana na wenzetu.” amesema Mangungu
Kocha huyo mwenye Umri wa Miaka 61 kabla ya kuvunja Mkataba na Vipers SC ndani ya Miezi 16 aliyokaa Klabuni hapo aliiongoza Vipers SC kushinda Michezo 43 kati ya 57 huku ikitoka sare 9 na kufungwa Michezo 6. Kwenye Michezo yote Vipers SC ilifunga Magoli 99.
Lakini pia amefanikiwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Nchini Uganda, Tuzo ya Kocha Bora wa Msimu Nchini Uganda pamoja kuiwezesha Vipers SC Kushiriki hatua ya Makundi ya Klabu Bingwa Barani Afrika Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa Kwa Klabu hiyo.