Kocha Mkuu wa Simba SC Robertinho amepongeza uwezo na uwajibikaji wa Wachezaji wake baada ya mchezo wa pili wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya CSKA Moscow.

Simba SC imemaliza kambi yake Dubai-Falme za Kiarabu ikiambulia matokeo ya sare ya 2-2, huku ikipoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Dhafra FC 1-0.

Kocha Robertinho amesema Kikosi chake kilionesha uwezo mkubwa wa kupambana dhidi ya CSKA Moscow wakati wa kipindi cha pili, na anajivunia hilo kwa sababu kuna vitu vya kiufundi ameviona.

Amesema kipindi cha kwanza kikosi chake hakikucheza vizuri sana na kupelekea kufungwa 2-0, lakini mabadiliko aliyoyafanya wakati wa kipindi cha pili yalifanikisha baadhi ya mambo kubadilika na kupata sare ya 2-2.

Amesema CSKA Moscow ilicheza vizuri na imetoa upinzani mkubwa kwa wachezaji wake ambao wamemaliza kambi kwa kujifunza mambo makubwa, watakayoyatumia kwenye michezo itakayowakabili.

“Tulicheza vizuri sana kipindi cha pili, wenzetu wana uzoefu wa kutosha, lakini tuliwazidi kimbinu na ndio maana tulifanikiwa kusawazisha kwa kufunga mabao mazuri.”

“Kwa hakika nimefarijika kuona wachezaji wangu wakicheza kwa kiwango kikubwa, ninaamini hili tulilojifunza hapa tutaliendeleza katika michezo itakayotukabili baada ya kurejea Dar es salaam.” amesema Robertinho

Mabao ya Simba SC ya kusawazisha katika mchezo huo yalifungwa na Mshambuliaji mzawa Habib Haji Kyombo, aliyeingia kipindi cha pili.

Simba SC inatarajia kurejea nyumbani Tanzania, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, utakaopigwa keshokutwa Jumatano (Januari 18), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kasisi wa Kikatoliki ateketezwa akiwa hai
Serikali yatoa ufafanuzi Airbus za ATCL