Ronald Koeman ameunga mkono maazimio ya mshambuliaji wake Wayne Rooney ya kutangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya England , kwa kusema ni maamuzi sahihi ambayo yamefanywa katika muda muafaka.
Ronald Koeman ambaye ni meneja wa klabu ya Everton, amesema Rooney amekua mtumishi mzuri wa taifa lake tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka 2003, baada ya kuzitumikia timu za taifa za vijana chini ya umri wa miaka 15, 17 na 19 tangu mwaka 2000.
Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi amesema ni wazi Rooney ameonyesha anataka kuelekeza nguvu zake katika klabu ya Everton, baada ya kurejea kwa mara ya pili akitokea Man Utd iliyomsajili mwaka 2004 alipokua The Tofees.
“Alikua na mazungumzo na kocha mkuu wa timu ya taifa ya England kabla ya kufanya maamuzi rasmi ya kutangaza kustaafu, kwa sababu aliamini ni wakati mzuri wa kuwajibika kisawa sawa akiwa na Everton,” Amesema Koeman. “Mara zote amekua ni mchezaji mwenye kufanya maamuzi katika muda sahihi, binafsi ninamuheshimu sana.
“Kama unafikia hatua ya kucheza katika kiwango cha juu na kushiriki kwenye michuano ya kombe la dunia na barani Ulaya mara kadhaa, una haja ya kufikia maamuzi kama aliyoyafanya mchezaji huyu, naamini itamsaidia sana katika kupanga mambo yake ya kucheza katika klabu ya Everton.
“Haimaanishi kama amechoka ama umri umetupa mkono, Rooney bado ana nguvu na umri wa kucheza soka upande wa timu ya taifa anao, lakini ameona muda uliopo ni bora akaelekeza akili yake kwenye klabu pekee na sio jambo lingine.
Rooney anatarajia kuwa sehemu ya kikosi cha The Toffees kitakachopambana leo kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya mtoano ya michuano ya Europa League, dhidi ya Hajduk Split nchini Croatia.
Hata hivyo kiungo Davy Klaassen na mshambuliaji Sandro Ramirez hawakusafiri na kikosi cha Everton, na tayari Koeman amethibitisha suala hilo katika mkutano na waandishi wa habari.
Amesema Klaassen anakabiliwa na majeraha ya mguu, ilihali Sando anaendelea kujiuguza majeraha ya kisigino.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Goodison Park juma lililopita, Everton waliibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.