Nahodha na Mshambualiji wa timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo amefikia Rekodi ya ufungaji bora wa muda wote kwa timu za taifa, iliyokuwa imewekwa na Mshambuliaji wa zamani wa Iran Ali Daei.
Ronaldo aliifikia rekodi hiyo usiku wa kuamkia leo, baada ya kuifungia Ureno mabao mawili ya Penati dhidi ya Mabingwa wa dunia timu ya taifa ya Ufaransa, kwenye michuano ya UEFA Euro 2020.
Mchezo huo ulishuhudia miamba hiyo ya soka Barani Ulaya ikifungana mabao 2-2 na kufuzu hatua ya 16 ya michuano ya UEFA Euro 2020, inayoendelea katika miji mbalimbali Barani Ulaya.
Mshambuliaji huyo wa klabu ya Juventus, amefikisha mabao 109 aliyoifungia timu ya taifa lake la Ureno tangu alipoanza kuitumikia mwaka 2003.
Baada ya kuifikia rekodi hiyo ya Ali Daei, Ronaldo anapewa nafasi kubwa ya kuandika rekodi mpya ya upachikaji mabao kwa timu za taifa, kutokana na kuendelea kuwa sehemu ya wachezaji wanaozitumikia timu zao za taifa kwa sasa.
Ali Daei, ambaye ameitumikia timu ya taifa ya Irani katika michezo 149, alifunga mabao 109, kati ya mwaka 1993 na 2006.
Mchanganuo wa mabao ya Ronaldo katika michuano tofauti akiwa na timu ya taifa ya Ureno.
Mchakato wa kufuzu Fainali za UEFA Euro – Mabao 31
Fainali za UEFA Euro – Mabao 13
Mchakato wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia – Mabao 31
Michezo ya Kimataifa ya Kirafiki – Mabao 19
Fainali za Kombe la Dunia- Mabao 7
Michuano ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya (UEFA) – Mabao 5