Mshambuliaji kutoka nchini Ureno Cristiano Ronaldo ametajwa kuwa nahodha wa kikosi cha Wachezaji wa ligi ya Saudi Arabia ‘Saudi All Stars Team’, kitakachoivaa PSG kesho Alhamis (Januari 19).
Ronaldo aliyejiunga na Klabu ya Al Nassir ya Saudi Arabia mwezi uliopita, baada ya kuvunja mkataba na Klabu ya Manchester United ya England, amejumuishwa kwenye kikosi hicho, ambacho kwa mara ya kwanza kitacheza dhidi ya Mabingwa wa Ufaransa katika mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki.
Ronaldo amepata Fursa hiyo, kutokana na uwezo wake wa kusakata kabumbu, ambao unamuwezesha kutumika kama kigezo kwa wachezaji wengine wanaounda kikosi cha ‘Saudi All Stars Team’.
Tayari Kikosi cha PSG kimewshawasili mjini Ryyadh-Saudi Arabia kwa mchezo huo, ambao utamkutanisha Lionel Messi na Mpinzani wake wa karibu Ronaldo kwa mara ya kwanza tangu msimu wa mwaka 2020/21.
Msimu huo Ronaldo akiwa Juventus FC ya Italia aliisaidia timu yake kuibuka na ushindi mnono wa magoli 3-0 dhidi ya FC Barcelona, iliyokuwa ikitumikiwa na Lionel Messi kabla hajatimkia PSG.
Mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya Hatua ya Makundi, ulishuhudia Nahodha huyo wa kikosi cha Ureno akifunga mabao mawili kwa mikwaju ya Penati.
Uwepo wa Lionel Messi na Ronaldo katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki utakaopigwa Uwanja wa King Fahd mjini Ryadh-Saudi Arabia, unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi duniani kuufuatilia mchezo huo.
Wakati huo huo Cristiano Ronaldo amekuwa Binaadamu wa kwanza kufikisha wafuasi (followers) Milioni 160 kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook. Pia ndiye mtu anayefuatiliwa zaidi kwenye mtandao wa Instagram akiwa na wafuasi Milioni 535, Wakati kwenye Twitter, ana wafuasi Milioni 107.2.