Kamati ya utendaji ya shirikisho la riadha (RT) inatarajia kukutana April 12 na 13 kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ya kimaendeleo ya shirikisho hilo.
Katibu mkuu wa RT Wilhem Gidabudai, amesema matayarisho ya kikao cha kamati ya utendaji yanakwenda vizuri na wanatarajia watakapomaliza, mchezo wa riadha utapata msukumo zaidi katika mpango wa maendeleo.
Didabudai hakuwa tayari kuweka wazi agenda kuu watakazokwenda kuzijadili, lakini alisisitiza suala la mendeleo na tathmini ya michuano ya dunia ya mbio za nyika iliyofanyika mjini Kampala nchini Uganda mwishoni mwa mwezi uliopita vitapewa kipaumbele.
“Tutajadili sana maendeleo kwa sababu tunataka kuona mchezo huu unaendelea na kuacha kasumba ya maneno bila vitendo, pia tutajadili ripoti ya Tathmini ya michuano dunia ya mbio za nyika iliyofanyika mjini Kampala nchini Uganda mwishoni mwa mwezi uliopita, japo hatukupata medali, lakini tumepiga hatua.” Alisema Gidabudai.
Katika hatua nyingine Gidabudai amesema kikao cha kamati ya utendaji ya RT pia kitafikia maamuzi ya mwisho kuhusu mwanariadha Ismail Juma ambaye alionyesha utovu wa nidhamu siku chache kabla ya timu ya taifa haijaingia kambini mkoani Arusha mwishoni mwa mwezi Februari, kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya mbio za nyika.
“Tayari ameshatumikia adhabu kwa mwezi mmoja sasa, uchunguzi wetu umebaini kuwa halikua kusudio lake kutoroka nchini, bali watu wanamzunguuka akiwepo kocha wake walimshauri vibaya.” Alisema
Ismail Juma aliondoka nchini bila ruhusa na kwenda nchini Marekani kushiriki michuano ya Marathon, jambo ambalo lilipokelewa kwa mshangao mkubwa na viongozi wa RT ambao waliarifiwa alikua anaumwa.