Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Antoine Griezmann ameshindwa kuweka wazi mpango wa kuondoka ama kubaki Atletico Madrid mwishoni mwa msimu huu, lakini amekataa kabisa kuhusishwa na mpango wa kuhamia kwa majirani zao Real Madrid.

Griezmann ametangaza msimamo huo, baada ya kubanwa na waandishi wa habari ambao walimuuliza kuhusu mustakabali wake, endapo ataamua kuondoka Atletico Madrid mwishoni mwa msimu huu.

Mshambuliaji huyo ambaye aliifungia bao la kusawazisha Atletico Madrid wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya Real Madrid siku ya jumamosi, amesema suala la kuondoka ama kubaki litabaki katika maamuzi yake, lakini kwa sasa anatambua ni mchezaji halali wa Vicente Calderon.

Amesema ni vigumu kueleza nini kitakachotokea kesho, lakini akawahakikishia waandishi wa habari kuwa, bado ana mkataba na Atletico Madrid na bado ana furaha kuendelea kufanya kazi klabuni hapo.

“Siwezi kusema lolote, lakini ninajihisi furaha kuendelea kuitumikia klabu yangu, sioni sababu ya kuanza kusema safari ya kuelekea mahala pengine mwishoni mwa msimu huu.

“Real Madrid ni klabu nzuri na ina mipango ya kuvutia, lakini sijawahi kufikiria kujiunga nayo kwa sababu naamini nilipo sasa kuna uwezo mkubwa wa soka kuliko huko mnamponiambia.” Griezmann aliwajibu waandishi wa habari.

Hata hivyo kauli ya Griezmann, huenda ikawa imetoa faraja kwa meneja wa Man Utd Jose Mourinho, ambaye kwa majuma kadhaa alitajwa kuwa katika harakati za kutaka kumuhamishia Old Trafford mwishoni mwa msimu huu.

Kutajwa kwa Real Madrid kwenye mkakati huo, ilionekana kuwa kikwazo kwa meneja huyo kutoka nchini Ureno, lakini msimamo wa Griezmann huenda ukawa umempa faraja ya kuamini anaweza kumpata endapo atatuma ofa nzuri.

Klabu nyingine zinazotajwa kumuwania Griezmann ni Man City pamoja na PSG.

RT Kuamua Hatma Ya Ismail Juma
CUF hali si Shwari, Maalim atoa tamko zito